UKUMUSHI KATIKA VITENZI VYA KISWAHILI
Kiswahili ni lugha ukumushi wa baada ya kikumushwa. Hata hivyo, kuna nyakati ambapo utaratibu huu hukiukwa. Kwa kutumia sintaksia ya vitenzi vya Kiswahili, thibitisha au pinga dai hili.
Swali hili imegawanyika katika sehemu kuu nne, sehemu ya kwanza utangulizi ambayo imebeba dhana za msingi katika kazi kulingana na wataalamu mbalimbali, kiini amabapo sehemu hii tumejadili swali pia hitimisho na marejeleo tuliyoyatumia katika kazi hii. Kwa kuanza na utangulizi dhana ya ukumushi imeelezwa kulingana na wataalamu mbalimbali kama ifuatavyo;
Khamisi na Kiango (2002:58) wanaeleza dhana ya ukumushi kuwa ni maneno ambayo siyo vivumishi kwa asili, lakini hufanya kazi kama vivumishi yaani kazi ya kukumusha (kuongeza sifa au taariafa muhimu. Wanaendelea kwa kusema kuwa vikumushi siyo vipashio vilivyo katika kiwango cha neon tu, bali ni pamoja na makundi ya maneno ambayo katika kiwango cha kirai au kishazi.
Chuo Kikuu Cha Oxford (2005) hueleza kuwa kikumushi ni neno ambalo linaweza kuwa kivumishi au kielezi ambacho kinaelezea neno au kundi la maneno mengine.
Philipo na Kuyenga (2017:80-81) wanazelea kuwa kikumushi ni neno lenye asili ya lugha za lugha za kibantu lenye maana ya “furushi” yaani kumusha au toa taarifa. Hivyo katika lugha vikumushi ni maneno yanayotoa taarifa zaidi juu ya meneno mengine mfano; nomino,kitenzi,kivumishi, na kielezi.
Hivyo kulingana na fasili hizo zilizotolewa na wataalamu mbalimbali tunaweza kusema kuwa kikumushi huweza kufasiliwa katika mawanda finyi na mawanda mapana, katika mawanda finyu kikumushi ni maneno yanayotoa taarifa ya ziada kuhusu nomino. Mfano; mtoto wangu, mtoto wa juma. Katika mawanda mapana kikumushi ni maneno yanayotoa taarifa ya ziada kuhusu aina nyingine yoyote ya maneno yaani nomino, kitenzi na kielezi. Mfano,
Aliyeimba kwa madaha
Anacheza vizuri sana
Katika data yetu hapo juu data A na B vikumushi ni kwa madaha na vizuri sana vya vitenzi aliyeimba na anacheza. Mazingira ya utokeaji wake ni baada ya nomino,kitenzi,vielezi.
Baada ya kuangalia dhana ya vikumushi kulingana na wataalamu mbalimbali, dhana ya vitenzi pia imejadiliwa na wataalamu kama ifutavyo;
Massamba (2004) anaeleza kuwa kitenzi ni kipashio kinachotoa taarifa kuhusu tendo lililofanyika, linalofanyika na au litakalofanyika.
Habwe na Karanja (2004:135) wanasema kitenzi ni maneno ambayo huwakilisha vitendo. Pia Mbaabu (1985) akinukliwa na Habwe na Karanja (kashatajwa) anavielezea vitenzi kama maneno yoyote yanayoonesha mambo yanayofanywa na watu, wanyama au vitu katika wakati Fulani. Anaendelea kueleza kuwa vitenzi huelezea hali za watu vitu na matukio.
Habwe na Karanja (2004:174), Obuchi (2015:148) wanatataja aina tano za vitenzi ambazo ni vitenzi vishirikishi, vitenzi elekezi, vitenzi vi so elekezi, vitenzi visaidizi na vitenzi vikuu. Wataalamu hawa wametofautiana katika matumizi ya istilahi kwani Habwe na Karanja wao wametumia istilahi ya vitenzi vikuu na Obuchi akitumia vitenzi halisi.
Hivyo basi kitenzi ni maneno yanayotumiwa kuarifu matukio, matendo na hali Fulani za watu, vitu katika wakati Fulani. Pia huuliza maswali, kutoa taarifa ama amri. Mfano, imba, cheka, omba, lia. Mfano
a.Juma anaimba vizuri.
b.Mwajuma anacheka vizuri.
Baada ya kufasili dhana za msingi katika swali letu zituatazo ni hoja zinazothibitisha kuwa Kiswahili ni lugha ya ukumushi baada ya kikumushwa. katika lugha ya Kiswahili vikumushi hutokea katika kategoria mbalimbali za maneno kama vile vielezi, nomino na vitenzi. Kwa kumrejelea Crif (1985) anasema kuwa kiswahili ni lugha ya ukumushi baada ya kukumushwa. Iwapo kiambajengo “A” cha kisintaksia kinakumusha kiambajengo “B” cha kisintaksia basi mfuatano wa viambajengo utakuwa ni “BA” ambapo “A” itakuwa kikumushi na “B” itakuwa kikumushwa, ingawa utaratibu huu huweza kukiukwa katika mazingira maalumu.
Habwe na Karanja (2004) wanaeleza vitenzi elekezi ni vitenzi huashiria kitendo na hali ambayo huruka mipaka na kuathiri maneno mengine ya sentensi. Maneno haya yanayoathiriwa huwa ni yambwa tendwa au tendewa. Vitenzi elekezi hudhihirisha ukumushi wa lugha ya Kiswahili baada ya kukumushwa kwa mifano ifuatayo,
Kitenzi kikuu na nomino
Juma anacheza mpira.
Mama anapika chakula.
Katika mifano apo juu vitenzi anacheza na anapika ni vikumushwa na nomino mpira na chakula ni vikumushi vya vitenzi hivyo.
Kitenzi kikuu na kielezi
Emanuel anasoma darasani.
Chausiku anaimba vizuri.
Katika mifano hapo juu tuna muundo kitenzi kikuu na kielezi, kitenzi anasoma na anaimba ni vikumushwa na vielezi darasani na vizuri ni vikumushi vya vitenzi hivyo.
Obuchi (2015:148) anaeleza vitenzi vishirikishihuonesha tabia au hali fulani kwa namna inayoonyesha umoja wa mambo fulani. Vitenzi hivi huashiria sifa au vyeo vya wahusika. Mifano ya vitenzi vishirikishi ni, si, yu li na zi. Vitenzi vishirikishi havina huwarifishaji mkamilifu kwa sababu hiyo hujalizwa na vikumushi ili kuwa na uharifishaji mkamilifu. Mifano ifuatayo hudhihirisha ukumushi wa lugha ya Kiswahili,
Kitenzi kishirikishi na nomino
Mwaisumo ni mwizi.
Zainabu si jambazi.
b.Kitenzi kishirikishi na kielezi
Musa yu kwetu.
Ndizi zi kikapuni.
Katika mifano hapo juu vitenzi vishirikishi ni, si, yu, na zi ni vikumushwa na vielezi mwizi, jambazi, kwetu na kikapuni ni vikumushi.
Kitenzi kishirikishi na kirai kihusishi utaratibu huu hutokea pale ambapo kirahi kihusishi kinatoa taarifa zaidi kuhusu kitenzi kishirikishi na hapo vitenzi vishirikishi huchukuliwa kama kikumushwa cha kikumushi kirai kuhusishi kama katika mifano ifuatayo.
Alikuwa kwa babamkwe.
Ni vya watoto
Katika mifano hapo juu vikumushwa ni alikuwa na ni na vikumushi vyake ni kwa na vya.
Mbali na kuangalia jinsi vitenzi vya Kiswahili vinavyokumushwa wakati mwingine utaratibu huu wa ukumushaji unakiukwa na vitenzi visoelekezi kwa sababu vinajitosheleza kimaana.
Habwe na karanja (2004:175) wanaeleza vitenzi visoelekezi ni vitenzi ambavyo haviitaji yambwa. Vitenzi hivi huwa vinakamilika kimaana katika matumizi yake. Mawazo haya yanaungwa mkono na Obuchi (2015) anaeleza vitenzi hizi havichukui yambwa kwani huwa vimekamilika katika maana zake. Mfano
a.Mtoto analia.
b. John amelala.
c. Mwansoka amefurahi.
Kwa kuhitimisha sintaksia ya vitenzi katika kuonyesha ukumushi na kikumushwa hutegemeana na uhusiano Kati ya vitenzi hivyo na maneno mengine, hata hivyo vitenzi ndio msingi mkuu wa sentensi na kwa wakati mwingine huweza kusimama Kama sentensi kamili kwa sababu huweza kuwa na muundo sahihi wenye viambata vyote licha ya kuwa Kuna baadhi ya viambata hivyo visionekane au kutajwa katika mazingira.
MAREJELEO
Chuo kikuu cha Oxford (2005). Advance learners dictionary. U.S.A: Oxford university press.
Habwe na karanja, (2004). Misingi ya sarufi ya Kiswahili. Nairobi: phoenix publishers Ltd.
Khamis, A. M na Kiango, J.G (2002). Utangulizi wa sarufi ya Kiswahili. Dar es salaam.
Massamba, D. P. B (2004). Kamusi ya isimu ya falsafa ya lugha. Dar es salaam: TUKI.
Obuchi, M. S (2015) Muundo wa Kiswahili ngazi na vipengele. Nairobi-kenya: printing services
limited.
Philipo, Z. T na Kunyenga, F.E (2017). Sintaksia ya Kiswahili. Nadharia za kisintaksia na
uchunguzi wa Kiswahili. Dar es salaam: karljamer publishers limited.
Comments
Post a Comment